Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Amirul-Mu’minin (a.s.) katika Nahjul-Balagha kuhusu thamani na athari za taqwa anasema:
اعْلَمُوا عِبَادَ اللَّهِ أَنَّ التَّقْوَی دَارُ حِصْنٍ عَزِیزٍ .... أَلَا وَبِالتَّقْوَی تُقْطَعُ حُمَةُ الْخَطَایَا
“Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Jueni kwamba taqwa ni ngome madhubuti isiyoweza kushindwa … Tambueni kwamba kwa kujilinda kwa taqwa, mizizi ya madhambi inaweza kung’olewa.” [1]
Sherehe:
Kama ambavyo mwanadamu anahitaji vazi la dhahiri kufunika mwili na heshima yake, vilevile anahitaji vazi kwa ajili ya kufunika uovu wa ndani, vazi la nje hulinda mwili dhidi ya baridi na madhara ya kidhahiri na pia huwa pambo la mtu, hali ya ndani ya mwanadamu nayo iko kwenye hatari, nayo inahitaji kupambwa kwa sifa za kimungu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuhadharisha kuhusu hatari hii kwa maneno yafuatayo:
یَا بَنِی آدَمَ لَا یَفْتِنَنَّکُمُ الشَّیْطَانُ
“Enyi wanaadam! Asiwafitinisheni nyie Shetani.” [2]
Japokuwa sisi hatumuoni shetani, yeye anatufahamu vyema. Anachunguza kila jambo dogo na kubwa la matendo yetu na daima anatafuta mwanya na nafasi ya kupenya katika nafsi na roho ya mwanadamu, Kama Qur’ani inavyosema:
إِنَّهُ یَرَاکُمْ هُوَ وَقَبِیلُهُ مِنْ حَیْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ
“Yeye (shetani) na kikosi chake wanakuoneni kutoka sehemu ambayo nyinyi hamuwaoni wao.” [3]
Kwa sababu hiyo akasema:
وَلِبَاسُ التَّقْوَی ذَلِکَ خَیْرٌ
“Na vazi la taqwa hilo ndilo bora zaidi.” [4]
Hii inaonyesha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka kumuwezesha mwanadamu kukabiliana na shetani — adui aliyeapa waziwazi — kwa kumpa silaha ambayo itamfanya yeye na genge lake washindwe kabisa kupenya katika nafsi ya mwanadamu.
Ni hiyo silaha ambayo Amirul-Mu’minin (a.s.) ameitaja kama “ngome madhubuti isiyoweza kushindwa.” Silaha inayoweza kukausha mizizi ya madhambi yote madhambi yanayomsogeza mwanadamu mbali na Muumba wake.
Rejea:
1. Nahjul-Balagha, khutba ya 157.
2. Suratu A‘rāf, aya ya 27.
3. Suratu A‘rāf, aya ileile.
4. Suratu A‘rāf, aya ya 26.
Imeandaliwa na Idara Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako